Muonekano mwingine व Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege wakati wa kikao hicho
Mkurugenzi
 Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege (kushoto) 
akiwa hoi wakati Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za 
Mashirika ya Umma (PAC), Deo Filikunjombe (kulia), akimshutumu kwa 
utendaji wake mbovu, uliojaa utapeli ambao Kamati hiyo iliugundua katika
 ziara nje ya Nchi ya kukagua kampuni za ukaguzi wa magari yanayoingizwa
 nchini. Filikunjombe alikuwa anazungumza hayo katika kikao cha kamati 
za Bunge za Hesabu za Serikali (POAC) na PAC cha kujadili utendaji wa 
Wizara ya Viwanda na Biashara, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege
 akizungumza na wanahabari baada ya sakata hilo, hata hivyo hakutaka 
kufafanua jambo lolote , hivyo kuamua kuondoka na kuwaambia kuwa 
wanahabari atakutana nao leo kuelezea kwa kina.
Makamu
 Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC), Deo
 Filikunjombe (kulia), akimshutumu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango
 Tanzania (TBS) Charles Ekelege (picha ya juu) kwa utendaji wake mbovu, 
uliojaa utapeli ambao Kamati hiyo iliugundua katika ziara nje ya Nchi ya
 kukagua kampuni za ukaguzi wa magari yanayoingizwa nchini. Filikunjombe
 alikuwa anazungumza hayo katika kikao cha kamati za Bunge za Hesabu za 
Serikali (POAC) na PAC cha kujadili utendaji wa Wizara ya Viwanda na 
Biashara, Dar es Salaam
Mbunge
 Lugora akielezea jinsi alivyoaksilishwa na ubabaishaji wa Ekelega, na 
kuamua kumrushia konde ambalo lilidakwa na Filikunjombe wakiwa Ughaibuni
 baada kamati kupewa sumu feki ya kampuni ya nje inayokagua magari 
yanayoingizwa nchini
Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya (CCM), akielezea jinsi alivyotapeliwa na wakala wa ukaguzi wa magari
Katibu
 Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko,Joyce Mapunjo (katikati),
 akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za 
Mashirika ya Umma (PAC), Deo Filikunjombe (kushoto) na Mwenyekiti wa 
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (POAC), John Cheyo baada ya kamati
 hizo kumtajia uozo wa ukaguzi wa magari unaofanywa na Shirika la 
Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na kampuni feki za nje ya 
Nchi,jana wakati wa vikao vya Kamati za Bunge, Dar EsSalaam.Picha na 
Mdau Richard Mwaikenda
--
KAMATI
 ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) imemlipua Mkurugenzi Mkuu wa 
Shirika la Viwango Nchini (TBS), Charles Ekelege baada ya kubaini kuwa 
shirika hilo lina ofisi hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi.
Imesema kutokana na hali hiyo fedha za ukaguzi zinazotolewa na wanunuzi 
wa magari, zinaishia mikononi wa wajanja huku ikisisitiza kuwa itaanika 
madudu mengine ya TBS katika kikao cha Bunge kinachoanza wiki ijayo na 
kwamba hali hiyo ndio chanzo cha kujazana kwa magari mabovu nchini. 
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Hesabu za Serikali, (PAC), Makamu
 Mwenyekiti POAC, Deo Filikunjombe alisema waligundua madudu hayo baada 
ya kamati yake kutembelea vituo vya ukaguzi wa magari nchini Singapore 
na mjini Hong Kong, China.
Wakati Filikunjombe akieleza hayo mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya 
Viwanda, Biashara na Masoko, Joyce Mapunjo, Ekelege alionekana kuishiwa 
nguvu na kupata mshangao. Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za 
Serikali, John Cheyo alisema a walilazimika kuwaita wajumbe wa POAC 
katika kikao hicho kwa kuwa suala hilo ni nyeti. “Tulikwenda Hong Kong 
na Singapore na tumegundua kwamba TBS ni wababaishaji, huwezi kuamini 
anachokifanya Mkurugenzi (Ekelege) huko nje”,
“Ninasema haya bila woga wowote na hata nikiwekewa sumu, wajumbe wengine
 wa kamati yangu watasema,” alisema. Alisema walipotembelea Hong Kong, 
waligundua kuwa ukaguzi wa magari haufanyiki na kwamba fedha 
zinazotolewa na wanunuzi zinaliwa na wajanja.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa kamati,Ekelege aliwapeleka katika ofisi 
hewa ambayo baadaye waligundua kuwa haikuwa ya ukaguzi wa magari. 
“Katibu (Mapunjo) ili ulinde heshima yako usimbebe Ekelege, tumekwenda 
Hong Kong na akatupeleka katika ofisi feki na tulipombana akasema kuwa 
aliomba kwa muda kuitumia ofisi hiyo,” alisema Filikunjombe. Alisema 
kampuni inayotumiwa na TBS kukagua magari nje ya nchi inapasaw ieleweke 
huku akifafanua kuwa wakati wakiwa Hong Kong, walinunua cheti feki cha 
TBS mtaani. “Huyu Ekelege si mkweli, ukaguzi wa magari haufanyiki sisi 
tumekwenda na kujionea wazi, ndio maana magari mengi yakifika hapa 
yanakuwa mabovu na gharama za usafirishaji na ukaguzi zinakuwa kubwa,” 
alisema Filikunjombe.
Kwa mujibu wa Filikunjombe baadhi ya watu waliowakuta katika kampuni 
hizo waliwaeleza kuwa Ekelege amekuwa akiwaeleza kwamba fedha za ukaguzi
 zinazopatikana wazitumie kununulia vifaa vya magari. Alisema 
walipokwenda Singapore pia hawakukuta kampuni ya kukagua magari na 
kwamba walipomuuliza Ekelege akashindwa kuwapeleka zilipo ofisi za 
ukaguzi wa magari. “Jamani mashirika yetu ya umma yananyonywa na wajanja
 wachache, fedha zinaliwa na wakati tupo huko tuliomba namba za simu na 
kupewa za uongo,” alisema Filikunjombe.
Alisema kama Mapunj) anambeba Ekelege, wao kama wabunge hawatakuwa 
tayari kuvumilia suala hilo huku akisisitiza kuwa wana mengi ya 
kuzungumza kuhusu mkurugenzi huyo. “Hayo ni machache sana kuna mengi 
ambayo kamati tumeyagundua katika ziara yetu na tutayaanika hadharani 
Dodoma,” alisema Filikunjombe.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugora 
alisema walipokuwa nchini humo alitaka kupigana waziwazi na Ekelege 
baada ya kugundua jinsi walivyokuwa wakidanganywa kama watoto wadogo. 
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ester Bulaya alisema a 
ripoti ya TBS inaonyesha kuwa ukaguzi wa magari ni Dola150 lakini ofisi 
hizo za ukaguzi zinataka zilipwe Dola300. “Mimi mwenyewe walitaka 
kunitapeli nilikuwa nataka kununua gari na wakanieleza niwatumie Dola300
 wakati kawaida natakiwa kulipia Dola150, nilipowaeleza wakasema wana 
mtandao mkubwa na hata niende wapi siwezi kuwakamata,” alisema Bulaya.
Mapema Cheyo aliiponda ripoti ya TBS ya mwaka 2011 na kueleza kuwa ina upungufu mkubwa.
“Ripoti ina upungufu, kwanza haina takwimu zinazoonyesha magari mangapi 
yalikaguliwa na ukaguzi uliingiza fedha kiasi gani na zilizobaki ni 
kiasi gani” alisema Cheyo. Alisema licha ya taarifa ya CAG kueleza kuwa 
zoezi la ukaguzi wa magari halikufanyika ipasavyo, bado ukaguzi wa kucha
 bandia na nywele uliendelea kufanywa na kampuni hizo hewa.
“Hata vitu vilivyokaguliwa na kuonekana kuwa havifai haijulikani viko 
wapi, haijulikani kama vimetupwa ama laa, hakuna ushahidi vilikuwa kiasi
 gani” alisisitiza. Alisema kuwa kutokana na hali hiyo kamati yake 
haitaipitisha ripoti hiyo huku akimwagiza Mapunjo kuandaa upya ripoti 
hiyo na kuiwasilisha mbele ya kamati yake kabla ya Februari 2 na iwe 
imekaguliwa na CAG.
“Hakuna haja ya kuendelea kubishana tunaitaka wizara mpaka kufika 
Alhamisi ijayo (Februari 2) tupate takwimu zote na ziwe zimekaguliwa na 
CAG,” alisema Cheyo. Cheyo alimweleza Mapunjo kwamba kabla ya kumalizika
 kwa kikao cha Bunge mjini Dodoma watakutaka na Waziri wa Viwanda 
Biashara na Masoko na Kamati ya PAC na POAC ili kulijadili kwa kina 
suala hilo.
“Pia tutamweleza Spika wa Bunge ili kuona kama suala hili tunaweza 
kulifikisha bungeni ili wabunge watoe maoni yao,” alisema Cheyo. Ekelege
 anena Baada ya kikao hicho kumalizika Mwananchi lilimtafuta Ekelege ili
 ajibu tuhuma hizo ambapo alisema kuwa hawezi kuzungumza lolote huku 
akitaka atafutwe leo ofisini kwake.
Huku akionekana kuwa na kigugumizi Ekelege alisema,“Kwa leo siwezi 
kusema lolote kwa kuwa sina data (vielelezo), kesho (leo) njoo ofisini 
kwangu nitakueleza kila kitu, ila kwa sasa siwezi kusema lolote” alisema
 Ekelege Kauli ya Wizara Kwa upande wake Mapunjo alisema kuwa hawezi 
kueleza chochote kwa kuwa hajaipata ripoti ya CAG na kusisitiza kuwa 
atakapoipata ripoti atatoa ufafanuzi.