SERIKALI
 kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeingia tena katika kashfa ya 
ufisadi wa matumizi mabaya ya rasilimali za umma, baada ya kubainika 
kuuza kinyemela sehemu yenye utajiri mkubwa wa makaa ya mawe Kiwira kwa 
kampuni ya Tan-Power Resources (TPR). Uamuzi
 huo unaelezwa na wachunguzi wa mambo kuwa utaathiri mradi wa kuzalisha 
umeme wa makaa ya mawe kwa kusababisha bei ya nishati itakayozalishwa 
eneo hilo kuwa ghali na italisababishia serikali hasara ya dola za 
Marekani 600 milioni sawa na Sh960 bilioni. Tuhuma
 hizo za ufisadi, ziliibuka kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za 
Mashirika ya Umma (POAC) na kuifanya iwaite maofisa wakuu wa Wizara ya 
Nishati na Madini kujieleza mbele yao, jana. Sehemu
 inayodaiwa kuuzwa ilitajwa kuwa ni mlima Kabulo, ambayo aliielezea kuwa
 ina utajiri mkubwa zaidi wa makaa ya mawe kuliko eneo jingine la 
Kiwira. Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe alithibitisha kamati yake kuwaweka 'kitimoto' maofisa waandamizi wa wizara hiyo. "Tumewaita
 ili watupe maelezo ya kina kuhusu suala hilo," alisema Zitto 
akilalamika; "Hili ni tatizo la kuchezea raslimali za nchi," Zitto
 ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Upinzani 
Bungeni alisema tukio hilo limekuja wakati ambao serikali imetakiwa 
kumiliki hisa zote za mradi huo ili kuhakikisha anapatikana mbia 
anayeweza kuendesha mradi huo kwa faida. Alisema
 mradi huo ambao ulikuwa unamililikiwa kwa pamoja kati ya serikali na 
kampuni ya Tan-Power Resourses, ulitakiwa kusimamishwa pia wafanyakazi 
walipwe haki zao. Lakini
 mpaka sasa, alisema wafanyakazi hawajalipwa ingawa mradi huo umesimama 
jambo ambalo linaendelea kuisababishia hasara serikali. Akizungumzia
 athari za kuuzwa kwa eneo lenye utajiri mkubwa wa makaa ya mawe, Mbunge
 wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alisema mradi wa umeme 
unaotarajia kuanzishwa, gharama yake itakuwa kubwa kutokana na malighafi
 kuzalishwa na kampuni nyingine. Ole
 Sendeka alisema Serikali ilikopa Benki ya Dunia dola za Marekani 600 
milioni sawa na Sh960 bilioni kwa ajili ya kuendeleza mradi huo lakini 
kwa kuuzwa sehemu ya Kiwira, serikali itapata hasara kwa kulipa fedha 
hizo na riba yake kwa mradi ambao unamilikiwa na kampuni binafsi.  Hadi
 jana jioni Mwananchi lilipoondoka katika ofisi za Bunge, watendaji wa 
Wizara walikuwa bado hawajawasilisha maelezo yao mbele ya kamati hiyo.
Historia ya Kiwira
Kiwira
 ni moja ya miradi ambayo Serikali imeiweka katika orodha ya kuzalisha 
umeme ili kuliokoa taifa kwenye uhaba mkubwa wanishati ya umeme. Waziri 
wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliwahi kuliambia bunge kuwa 
Serikali imeamua kubeba mzigo wa mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira ili 
kuhakikisha kuwa unaleta tija kwa Taifa. Kampuni ya TPR inadaiwa 
kumilikiwa na  familia ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri wa 
zamani Nishati na Madini, Daniel Yona. Ngeleja alikuwa ameliambia bunge 
kuwa baada ya uamuzi huo, serikali imeanza mchakato wa kupata uratatibu 
muafaka wa kuendesha mradi huo kama ilivyokusudiwa kwa kuangalia fursa 
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuingia mkataba wa uendeshaji na kampuni 
itakayopewa mamlaka ya kujenga na kuuendesha. “Chini ya mkataba wa 
uendeshaji, mkandarasi atapewa jukumu la kujenga uwezo wa mashirika ya 
Stamico (Shirika la Madini) na Tanesco ili kuyawezesha kumiliki na 
kusimamia mradi huo,” alisema. Kwa mujibu wa Ngeleja, hatua ya awali ya 
mpango wa serikali kuanza kuundesha mradi huo zilikuwa zimeanza kwa 
kuhakikisha kuwa wafanyakazi waliopo wanalipwa haki zao zote na 
kuwawekea mazingira mazuri ya kuendelea na kazi. “Serikali pia 
imezungumza na serikali rafiki ya China iliyoanzisha na kuendesha mradi 
huo ili kupata mkopo wa kuufufua na kuhakikisha mradi wa kuzalisha umeme
 wa MW 200 unakamilika mapema iwezekanavyo,” alisema Akizungumzia suala 
la Rais Mstaafu Mkapa ambaye aliomba kumiliki hisa 200,000, kupitia 
kampuni yake ya ANBEN Limited, Ngeleja alisema kuwa kiongozi huyo wa 
zamani alinyang’anywa hisa hizo Januari 10 mwaka 2005 baada ya kushindwa
 kuzilipia.  “Mheshimiwa Spika, tarehe 10 Januari, 2005, (Siku 13 tangu 
kuanzishwa kwa TPR), ANBEN Limited iliondolewa kuwa miongoni mwa 
wamiliki wa hisa kwa vile haikuweza kulipia hisa ilizokuwa imechukua 
wakati wa usajili wa TPR. Hivyo wamiliki wa TPR waliobaki walikuwa ni 
DevConsult International Ltd, Universal Technologies Ltd, Choice 
Industries Ltd na Fosnik Enterprises Ltd zote zikiwa na hisa 200,000,” 
alisema Ngeleja. Wakati huo huo, Zitto alisema jana waliwahoji maofisa 
waandamizi wa Wizara ya Uchukuzi kwa kile kilichodaiwa ni Shirika la 
Ndege Tanzania (ATCL) kuingia kwenye mikataba inayoliingizia taifa 
hasara. Zitto hakutaja mambo yaliyofanywa na ATCL na kuisababishia 
hasara serikali lakini taarifa zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa 
linatakiwa kuilipa kampuni ya kigeni dola za Marekani 36 milioni. Fedha 
hizo zinadaiwa kuwa zilitolewa kwa ajili ya kukodisha ndege ambayo hata 
hivyo haikuwahi kufanya kazi nchini.
 
 
No comments:
Post a Comment