Kambi za wafugaji Sudan Kusini
Maafisa wa serikali katika Sudan
 Kusini wanasema watu wasiopungua 40 wameuwawa na kundi la watu wenye 
silaha waliokwenda kuiba mifugo.
Baadhi ya taarifa zinasema idadi ya watu 
waliouwawa ni zaidi ya 100 kwenye uvamizi, huo uliotokea kwenye kambi 
moja katika jimbo la Warrap.
                     
Waziri
 wa mambo ya ndani wa Sudan Kusini ameilaumu serikali ya Sudan kwa 
kuwapa silaha washambuliaji hao, ambao ni kundi la wapiganaji kutoka 
jimbo jirani la Unity.
Mvutano umeendelea kuwepo tangu Sudan Kusini ilipojitenga kutoka Sudan mwezi Julai, kufuatia vita vilivyochukua miaka mingi.
Afisa ammoja katika jimbo la Warrap ameambia 
gazeti la Sudan Tribune linaloandikiwa mjini Paris kwamba vijiji 
vinavyokaliwa na watu wa jamii ya Luac Jang katika wilaya ya Tong 
mashariki walishambuliwa Jumamosi alfajiri.
Spika wa bunge Madot Dut Deng amesema ameambiwa na maafisa kwamba zaidi ya watu 76 wameuwawa, na wengine hajulikani walipo.
Afisa mwingine katika jimbo hilo aliambia gazeti hilo watu katika eneo lililoshambuliwa wanasema waliouwawa ni zaidi ya 100.
Waziri wa mambo ya ndani Alison Manani Magaya 
amesema mashambulizi hayo yaliendeshwa na kundi la wapiganaji kutoka 
jimbo jirani la Unity.
"kundi hili lilipewa silaha na serikali ya Khartoum," aliambia gazeti la AFP, lakini hakutaja ni kundi gani.
Sudan Kusini ilipata Uhuru tarehe 9 Julai mwaka 2011 kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe na Sudan.
Tatizo lililochangia mzozo hadi sasa ni kwamba silaha nyingi zimezagaa.
Silaha hizo zinatumika katika mapigano ya 
kikabila, ambayo mara nyingi yanahusu mifugo kutokana na umuhimu wake 
miongoni mwa jamii nyingi katika Sudan Kusini.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon siku
 ya Jumapili alitoa wito kwa viongozi wa Sudan na Sudan Kusini kufanya 
makubaliano kuhusu namna ya kugawana utajiri unaotokana na mafuta, 
ambayo husababisha mvutano baina ya nchi hizo mbili.
 
 
No comments:
Post a Comment