Wakati
 Tanzania ikiwa imeridhia mkataba wa kimataifa wa kutekeleza na kulinda 
haki za watoto na kusimamia kwa karibu ulinzi wa haki za binadamu, sasa 
serikali ina kila sababu ya kuangalia haki za watoto walioko gerezani 
kwa makosa ya wazazi wao.
 
 Miongoni mwa haki ambazo serikali inapaswa kuchunguza kwa undani na 
kubainisha kisa kilichosababisha mtoto mdogo wa kike wa miezi sita , 
Azra Vuyo Jack, ajikute yeye na wazazi wake wakiwa katika mahabusu ya 
gereza la Ruanda jijini Mbeya wakikabiliwa na tuhuma za kukutwa na dawa 
za kulevya.
 
 Azra ambaye kwa jina la utani, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na 
Mbeya yetu huko gerezani anaitwa Merryciana au bibi jela jina ambalo 
limezoeleka zaidi mbali ya jina lake halisi alilopewa na wazazi wake la 
Azra   .
  
 Mtoto huyo wa kike aliendelea kukua katika tumbo la mama yake akiwa 
gerezani, hatimaye alizaliwa salama Julai 15 mwaka jana katika hospitali
 ya wazazi meta.
  Mama yake ni Anastazia Cloete (27) mwenye asili ya kizungu, raia wa Afrika ya kusini
 
 Cloete alikamatwa mwaka juzi, Novemba katika mpaka wa Tanzania na 
Zambia , mji mdogo wa Tunduma akiwa mjamzito na kutupwa mahabusu katika 
gereza hilo hali iliyomfanya aendelee  kulea ujauzito wake.
  Uchunguzi wa kina uliendelea kufanywa na madaktari wa hospitali hiyo hadi alipojifungua salama.
  
 Uchunguzi wa tukio la mtoto huyo hadi sasa umezusha mwendelezo wa 
harakati za kihabari na wanaharakati wa haki za binadamu kuona umuhimu 
wa kuondolewa kwa mtoto huyo ambaye kwa muda wote tangu azaliwe amekuwa 
akitumia maziwa ya kopo na hanyonyeshwi na mama yake mzazi.
 
 Mmoja wa ya wasamaria wema aliyejitolea kuwahudumia watuhumiwa hao 
waliyokumbwa na tuhuma za kukutwa na dawa hizo ni Emily Mwaituka ambaye 
amekuwa akifanya kazi kubwa ili kuhakikisha mtpto anakuwa na afya nzuri 
kwa kununuliwa makopo mawili ya maziwa kila wiki tangu alipozaliwa 
julai, mwaka jana.
 
 Mwaituka anasema amekuwa akinunua kopo moja la maziwa ya unga aina ya 
SMA 1 ambalo huuzwa sh 26000 na anapaswa kununua makopo mawili ili 
kuweza kumudu mahitaji ya mtoto huyo wa kike ambaye hanyonyi maziwa ya 
mama yake mzazi anayesubiri hatima ya kesi inayomkabili akiendelea kuwa 
mahabusu kwenye gereza la Ruanda jijini Mbeya.
 
 Uchunguzi uliofanywa na Mbeya yetu  umegundua kuwa Cloete aliyekuwa 
akisoma nchini kwao katika chuo cha Capetech alijifungua mtoto wa kike 
miezi sita iliyopita baada ya kushikwa uchungu akiwa mahabusu na 
kukimbizwa hospitali ya wazazi ya meta.
 
 Cloete ambaye amekuwa akitumia majina mawili kwani alipolazwa katika 
hospitali hiyo aliandikishwa jina la Anastazia Elizabeth wakati 
alifikishwa hospitalini hapo kwa uchunguzi akiwa mjamzito Januari 14 
mwaka jana na kufunguliwa jarada la matibabu lenye namba 46 – 26 – 83.
 
 Uchunguzi umebaini kuwa raia huyo wa afrika ya kusini na mumewe , Vuyo 
Jack ( 31 ) waliokamatwa mpakani hapo, aligundulika kuwa mjamzito 
alipokuwa mahabusu na kuanza kupatiwa matibabu sahihi yaliyosaidia 
ujauzito wake kukua vizuri.
 
 Habari za ndani zinadai kuwa kwa muda wote huo baada ya ujauzito wake 
kugundulika alikuwa akipatiwa matibabu chini ya uangalizi wa madaktari 
na alipofikia  hatua za mwisho mjadala mzito ulifanywa na jopo la 
madaktari walioonyesha mashaka kuwa asingeweza kujifungua kwa njia ya 
kawaida na kutakiwa afanyiwe upasuaji.
 Imeelezwa
 kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika hospitali hiyo Peter
 Msafiri , alipofanya uchunguzi alibaini kuwa raia huyo hapaswi 
kufanyiwa upasuaji kwa vile alikuwa na uwezo wa kujifungua bila 
matatizo.
 
 Dk Msafiri alipohojiwa anasema Cloete alijifungua salama ingawa 
walitaka kumfanyia upasuaji lakini alipinga hatua hiyo na kudai kuwa 
anaweza kujifungua salama kwa njia ya kawaida.
 
 Baadhi ya wauguzi wa hospitali hiyo ambao hawakutaka majina yao kutajwa
 walidai kuwa raia huyo wa Afrika ya Kusini alijifungua mtoto wa kike na
 kwamba mama yake akiwa mahabusu amekataa kumyonyesha kwa madai kuwa 
hapati mlo wa kutosha unaomuwezesha kutoa maziwa ya kutosha kwa ajili ya
 mwanae.
 
 Cloete alilazwa hapo kwa ajili ya uchunguzi , hamnyonyeshi mtoto wake, 
kweli amejifungua mtoto mzuri wa kike, amesema kuwa hawezi kumnyonyesha 
na  anamlisha maziwa ya kopo akidai kuwa akinyonyesha atakosa nguvu kwa 
kuwa mahabusu alikowekwa hapati lishe bora anadai muuguzi mmoja.
 Miongoni
 mwa wanaharakati wa haki za binadamu walioguswa na habari za mtoto huyo
 kuendelea kukaa mahabusu na mama yake kulimgusa. Mchungaji William 
Mwamalanga, anasema kuwa kitendo cha mtoto huyo kuishi katika mazingira 
hayo hakuendani na haki za binadamu ambazo Tanzania imeridhia kwenye 
umoja wa mataifa.
 
 Mwamalanga anasema yeye na wanaharakati wenzake wanaandaa mpango 
maalumu wa kupigania haki ya mtoto huyo na kuhakikisha kuwa anaondolewa 
mahabusu baada ya kubainika kuwa amekuwa hanyonyeshwi na mama yake mzazi
 tangu alipozaliwa kwa madai kuwa hawezi kumnyonyesha kutokana na lishe 
duni anayopata akiwa mahabusu.
 
 Nakushukuru sana kuzisoma taarifa hizi, tunajiandaa ili kuona njia 
sahihi inayoweza kutusaidia kumtoa mtoto huyo mahabusu na kuiomba 
serikali iangalie kwa undani shauri hili kupitia kwa mwendesha mashtaka 
mkuu wa serikali ili kujua haki na stahili za mtoto huyo mchanga 
vinginevyo tunakiuka haki za watoto na binadamu ambazo Tanzania 
imeridhia kuzitekeleza, anasema Mwamalanga.
 
 Kumbukumbu za tukio hilo tulizonazo zinaonyesha kuwa raia hao wawili wa
 Afrika ya Kusini, waliokuwa wakiishi mtaa wa 2A Valley Road – 
Schaapkraal – Capetown walikamatwa na kilo 42 .5 za dawa za kulevya 
Novemba 18 mwaka juzi katika mpaka wa Tunduma na kufunguliwa – jalada 
namba TDM/IR/1763/2010.
 
 Katika tukio hilo ambalo Vuyo na Cloete walinaswa na dawa hizo 
walizozificha kwenye gari aina ya Nissana Hard body yenye namba za 
usajili CA – 508 – 656 lililokuwa likimilikiwa na Vuyo Jack waliokuwa 
wakitokea mkoani Morogoro kuelekea Afrika ya Kusini, Cloete alikuwa 
akisoma katika chuo cha Capetech.
 
 Kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo zimethibitishwa na Mkemia Mkuu wa
 Serikali dawa hizo za kulevya ni paketi 26 za cocaine zenye uzito wa 
kilo 28.5 paketi tatu za Heroine zenye uzito wa kilo 3.25 na paketi nane
 aina ya Morphine zenye uzito wa kilo 3.25, madawa hayo yote yanathamani
 ya zaidi ya sh bilioni 1.2.
 
 


No comments:
Post a Comment